
Rais Jakaya Kikwete
TANZANIA imeendelea kusisitiza kuwa, Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi, Madiwani na Masheha unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu utafanyika kwa amani na utulivu ambapo Watanzania watakuwa na uhuru wa kupiga kura bila woga kuwachagua viongozi wanaowataka.
Rais Jakaya Kikwete amesema furaha aliyonayo kumaliza salama kipindi chake cha uongozi na kujiandaa kukabidhi madaraka kwa rais ajaye, nchi bado ikiwa na umoja na mshikamano wa hali ya juu. Rais Kikwete ameyasema hayo Ikulu, Dar es Salaam alipokutana na mabalozi wanne wapya wa nchi mbalimbali waliofika Ikulu kuwasilisha hati zao za utambulisho.
“Kampeni zinakwenda vizuri na tunategemea uchaguzi mkuu utakuwa wa amani na Watanzania watapata nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka,” Rais Kikwete amewaeleza mabalozi hao katika nyakati tofauti mara baada ya kupokea hati zao na kufanya nao mazungumzo.
Rais Kikwete ametumia nafasi hiyo kuwaeleza mabalozi kuhusu hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Mabalozi waliowasilisha hati zao jana tayari kuanza kuziwakilisha nchi zao Tanzania ni Florence Tinguely Mattli wa Uswisi, Yesmin Eralp wa Uturuki, Pekka Juhani Hukka wa Finland na Katarina Rangnitt wa Sweden.
Rais Kikwete pia amewahakikishia mabalozi hao kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano mwema baina yake na nchi hizi ambazo ni rafiki na washirika wake wa maendeleo kwa miaka mingi.
0 comments:
Post a Comment