Suleiman Said Suleiman Wakati wa Uhai wake.
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Suleiman Said Suleiman amefariki dunia akiwa katika mazoezi ya kuogelea katika Bahari ya Hindi, eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mauti yalimkuta jana asubuhi baada ya kukosa nguvu wakati akiwa anaogelea.
Mkurugenzi wa Sheria wa TAA anayeshughulikia pia Uhusiano, Ramadhan Maleta, alisema ilikuwa ni kawaida ya Suleiman kufanya mazoezi ya mwili kila siku kabla ya kwenda kazini.
Alisema jana kati ya saa 12:00 na saa 1:00 asubuhi, akiwa anaogelea mmoja wa aliokuwa ameongozana nao, aligundua kuwa amekosa nguvu akiwa majini.
“Akaanza kumsaidia akiwa na wenzake ambao waliomba msaada kumtoa majini lakini wakagundua kuwa alikuwa ameshapata athari,” alisema Maleta.
Alisema walimkimbiza Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini kabla ya kufika walibaini kutokuwa na uhai.
Maleta alisema wafanyakazi wa TAA kwa ujumla wanasikitika kutokana na msiba huo, kwani Said alikuwa mtu wa mfano mwenye utaalamu wa viwanja vya ndege akiwa mhandisi mwenye ujuzi mkubwa.
Alisema alikuwa kiongozi mwenye upendo asiyekuwa na majivuno na kutokana na kuwa na roho nzuri na ukaribu na wafanyakazi, aliwatambua wafanyakazi wote wa TAA nchi nzima kwa majina.
Maleta alisema Mkurugenzi huyo ametumikia TAA kuanzia miaka ya 1970, akisimamia miradi mbalimbali ya uimarishaji na uboreshwaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini.
Alisema atakumbukwa daima kwa upanuzi wa uwanja wa Terminal 3.
Alisema katika ujenzi huo, alifanikisha kumaliza utata na kuhakikisha anapatikana mkandarasi ambaye amewezesha ujenzi kufikia mahali pazuri. Kwa mujibu wa Maleta, Suleiman ameacha mjane na watoto watatu.