Saturday, 16 January 2016

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani(NECTA),Charles Msonde.

IKIWA wanafunzi 324,068 ambao ni asilimia 89.12 wakipata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kuendelea na kidato cha Tatu, ufaulu wa masomo ya hisabati, fizikia, kemia na biashara uko chini ya wastani.
Aidha, wanafunzi 39,567 ambao ni asilimia 10.9 wameshindwa kupata alama za kuwawezesha kuendelea na masomo yao wakati mwaka 2014 wanafunzi 375,434 sawa na asilimia 92.66 walipata alama za kuendelea na masomo ya Kidato cha Tatu.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde alipokuwa akitan gaza matokeo ya upimaji wa kitaifa wa Kidato cha Pili.
Alisema kati ya wanafunzi 324,068 ambao wamepata alama za kuendelea na masomo, wanafunzi 155, 667 ambao ni asilimia 42.80 wamepata ufaulu mzuri wa kiwango cha juu (Distinction), Ufaulu wa daraja la pili (Merit) na ufaulu wa daraja la tatu (Credit) wakati zaidi ya nusu (wanafunzi 168,401) wakipata daraja la nne la ufaulu (Pass) .
Kuhusu ufaulu wa masomo, Msonde alisema ufaulu katika masomo ya msingi ya kiswahili, biashara na kemia umepanda kidogo ukilinganisha na mwaka 2014 wakati ufaulu wa masomo ya Uraia, Historia, Jiografia, Kiingereza, Fizikia, Hisabati na Utun zaji vitabu (Book-Keeping) umeshuka kidogo ukilinganisha na mwaka 2014.
”Somo lililofanyika vizuri zaidi ni Kiswahili ambapo asilimia 86.34 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamefaulu na somo lenye ufaulu wa chini zaidi ni Hisabati ambalo linaufaulu wa asilimia 15.21,” alisema.
Msonde aliongeza kuwa juhudi za makusudi zinahitajika kuendelea kufanyika ili kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo ambayo yako chini ya wastani na kuyataja kuwa ni hisabati, fizikia, kemia na biashara.
Akizungumzia shule zilizofanya vizuri alisema ni Mwanza Alliance, Alliance Girls na Alliance Rock Army (Mwanza), St Francis Girls (Mbeya), Bethel Sabs Girls Mafinga (Iringa), Shamsiye, Feza Girls, Feza Boys na Canossa (Dar es Salaam) na Don Bosco Seminary ya Iringa.
Alizitaja shule 10 za mwisho na kuwa mikoa ya Tanga na Mtwara ndio imeongoza kuwa na shule ambazo hazijafanya vizuri. Shule hizo za mwisho ni Michenjele (Mtwara), Furaha (Dar es Salaam), Mdando, Mlongwema na Kwai (Tanga), Lionja (Lindi), Mkoreha (Mtwara), Mlungui (Tanga), Makong’onda (Mtwara) na Kwaluguru (Tanga).
Msonde aliwataja wanafunzi waliofanya vyema kwa kuangaliwa wastani wa pointi (GPA) kuwa ni Lineth Christopher (St. Aloysius Girls), Jerry Panga( Marian Boys) na Rhobi Simba (Marian Girls) Colin Emmanuel (Feza Boys), Nickson Maro (Magnificat), Diana Mwakibinga (Morning Stars), Elisha Peter (Buswelu), Gaudencia Lwitakubi (Alliance Girls), Fuad Thabit (Feza Boys) na Geraldina Kyanyaka (Canossa) Wasichana 10 bora ni Lineth, Rhobi, Diana, Gaudencia, Geraldina, Renata Chokola (St.Aloysius Girls), Happyness Mwailunga (Canossa), Monica Tesha (St.Aloysius Girls), Judith Amos (Precious Blood) na Amina Khalfani (Feza Girls).
Wakati wavulana 10 bora ni Jerry, Colin, Nickson, Elisha, Fuad, Mwinangwa Chibunde (Mwanza Alliance), Baraka Muhammed (Eagles), Joshua Kafula (Libermann Boys), Emmanuel Magombi (Morning Stars) na Frank Charles (Marist Boys)
Categories:

0 comments:

Post a Comment