BENKI YAZINDUA MPANGO WA KUINUA BIASHARA
BENKI ya NBC imezindua mpango wa biashara kwa kujikita kwenye sekta za kilimo, usafirishaji, uzalishaji mali viwandani, mawasiliano na ufadhili wa biashara za ndani na nje ya nchi.
![Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Tanzania, Edward Marks (kulia), akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhelm Meru katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Huduma ya Biashara ya Kati ya benki hiyo, Dar es Salaam juzi. Anayeshuhudia ni Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo, Nehemiah Mchechu na Mjumbe wa Bodi ya NBC, Anthony De La Rue (kushoto). (Na Mpigapicha Wetu).](http://habarileo.co.tz/images/Non-Frequent/salimiana.jpg)
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhelm Meru aliipongeza NBC kwa kuanzisha mpango huo.
Dk Meru aliyekuwa mgeni rasmi, alisema utasaidia kwa kiwango kikubwa kukuza biashara na kuinua wajasiriamali ambao ni tegemeo la maendeleo ya uchumi nchini.
“Nimefarijika zaidi kuona sekta ya viwanda ni moja ya sekta zinazolengwa na huduma hii hivyo uzinduzi wa huduma hii naamini utaleta mafanikio kwa wajasiriamali na wafanyabiashara katika kuboresha na kuimarisha shughuli za kiuchumi wanazozifanya hapa nchini,” alisema Meru.
Alisema hivi sasa serikali imejielekeza katika kujenga uchumi wa viwanda na washiriki wakubwa katika kutimiza lengo hilo.
“Suala la upatikanaji wa mitaji ambayo itakuwa ni sehemu ya mpango huu uliozinduliwa limekuwa ni changamoto kubwa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati na kuwalazimisha kutopiga hatua katika biashara zao,” alisema.
Aliendelea, “ni mategemeo yangu kuwa huduma hii itawawezesha wajasiriamali wengi kushiriki katika ujenzi wa viwanda nchini, nikiri tu kwamba huduma hii imekuja katika wakati mwafaka,” alibainisha Katibu mkuu huyo.”
Alipongeza benki nchini kwa mabadiliko wanayoyafanya katika kuandaa programu maalumu kwa ajili ya wajasiriamali, huku akiagiza ziangalie uwezekano wa kuboresha viwango vya mikopo.
Akizungumza mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Edward Marks alisema huduma hiyo siyo tu inasaidia wafanyabiashara kwenye sekta za kilimo, viwanda, usafirishaji, na mawasiliano, bali inatoa huduma ya bidhaa zinazowafaa wafanyabiashara wanaohitaji mitaji ya kibiashara, ufadhili wa biashara za ndani na nje, fedha za kigeni na huduma za bima.
Mwenyekiti wa Bodi ya NBC, Nehemiah Mchechu amewaasa walengwa kutumia fursa ya huduma hiyo akisisitiza kuwa itawapa nafasi ya upatikanaji wa mikopo kwa muda mfupi zaidi, ufadhili wa kibiashara ya ndani na nje na ushauri wa kibenki.
Kwa mujibu wa Mchechu, wateja wa NBC watakaonufaika na huduma hiyo watapatiwa fursa kukutanishwa na wateja, wafanyabiashara wengine wakubwa zaidi ambao wamefanikiwa kujenga biashara zao kwa njia mbalimbali kupitia klabu maalumu.
0 comments:
Post a Comment