SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeanza majaribio ya umeme wa nishati mbadala ya upepo katika vijiji tisa, vinavyotekeleza mradi huo unaolenga kutoa nafuu kwa wananchi.
Meneja wa mradi wa nishati mbadala, Maulid Shirazi, alisema mradi huo umeanza kwa majaribio katika maeneo tisa ya Unguja na Pemba.
Alisema mradi huo ambao unafadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya kwa gharama ya Sh bilioni tatu, unatekelezwa katika maeneo ya Kiuyu Mbuyuni, Micheweni Pemba.
Alitaja maeneo ya Unguja ambapo mradi huo umeanza majaribio yake kuwa ni pamoja na Makunduchi, Uroa na Matemwe Mbuyyu tende. “Huu ni mradi unaofadhiliwa na jumuiya ya Ulaya ukiwa na malengo ya kupunguza gharama kubwa za nishati ya umeme unaozalishwa Tanzania Bara,” alisema.
Meneja wa Shirika la Umeme Pemba, Salum Masoud alisema kuwepo kwa mpango wa nishati mbadala wa umeme utapunguza gharama kubwa ya matumizi ya nishati hiyo kutoka kwa wananchi wa kawaida.
Alisema mradi wa nishati mbadala wa umeme kwa kutumia nguvu za upepo kwa sasa upo katika majaribio ambapo matumaini makubwa ni kuleta mafanikio.
Mradi wa nishati mbadala wa kutumia nguvu za upepo ulizinduliwa na Makamu wa pili wa rais, Balozi Seif Ali Iddi katika eneo la Kiuyu, Pemba kwa kuwataka wananchi kutumia huduma hiyo kupunguza gharama kubwa ya matumizi ya umeme wa kawaida.
Visiwa vya Unguja na Pemba vinategemea uzalishaji wa umeme kutoka Tanzania Bara, ambapo kwa muda mrefu serikali ipo katika utafiti wa nishati ya umeme mbadala.
0 comments:
Post a Comment