![](http://www.thecitizen.co.tz/image/view/-/2521936/highRes/875481/-/maxw/600/-/142tyge/-/muhongo.jpg)
Waziri wa Nishati na Madini,Mh.Sospeter Muhongo.
WATANZANIA 1,600 wa Mkoa wa Ruvuma wanatarajiwa kupata ajira katika hatua za awali za maandalizi ya uchimbaji wa madini ya urani wilayani Namtumbo.
Aidha, Watanzania 700 wanatarajiwa kupata ajira za kudumu baada ya shughuli za kuchimba madini hayo kuanza, baada ya utafiti wa madini hayo kufanywa na Kampuni ya MANTRA katika eneo la hifadhi ya Selou.
Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipotembelea mradi wa kufua umeme wa majenereta wilayani hapa mkoani Ruvuma.
“Hii ni neema nyingine kwa wakazi wa Ruvuma na wilaya ya Namtumbo. Iko wazi lazima Watanzania wanufaike na ajira katika utekelezaji wa mradi huu. Hatua za awali za mradi zitachukua hadi miaka miwili kabla ya mradi kuanza kutekelezwa,” alisema.
Akizungumzia suala la umeme kwa wakazi wa Namtumbo, Profesa Muhongo aliwahakikishia wakazi hao kuwa, ahadi ya Mbunge wa Namtumbo, Edwin Ngonyani bado iko pale pale na kwamba umeme utafika mapema tofauti na kama alivyoahidi mbunge wao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambugu alisifu jitihada zinazofanywa na wizara kuhakikisha taifa linakuwa na vyanzo vingi vya kuzalisha umeme na kueleza kuwa, mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe wa Ngaka utakuwa na manufaa makubwa si kwa mkoa wa Ruvuma tu, bali kwa taifa zima.
“Tuna imani na jitihada za waziri na wananchi wa Ruvuma, wanausubiri sana mradi huu. Tunaamini kuwa utekelezaji wake utaubadilisha mkoa wa Ruvuma,” Mwambungu alisema.
Akieleza kuhusu mradi wa madini ya urani, Mwambungu alisema kuwa tayari hatua za msingi za utekelezaji wa mradi huo zimekamilika na kinachosubiriwa ni taratibu za kusaini mikataba, (Mining Development Agreement- MDA).
Madini ya urani ni moja ya chanzo cha kuzalisha umeme na nishati yake inatajwa kuwa rafiki wa mazingira.
Baada ya kutembelea mradi wa majenereta, Waziri Muhongo alitembelea ofisi mpya ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Perahamiho ili kuhakikisha kwamba ofisi hizo zinaunganishwa na nishati ya umeme.
Baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi kutembelea miradi ya uzalishaji umeme na maeneo ya utafiti ya makaa ya mawe Mkoa wa Njombe na Ruvuma, Profesa Muhongo ataendelea na ziara kama hiyo mkoani Mbeya.
0 comments:
Post a Comment