![](http://www.habarileo.co.tz/images/resized/images/profs-muhongo_210_120.jpg)
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesisitiza kuwa tarehe iliyopangwa kati yake na Mameneja wa Tanesco nchi nzima kuhakikisha inawaunganishinia umeme wateja waliolipa kwa kipindi kirefu, ikiwemo kukamilisha matatizo ya LUKU iko palepale.
Profesa Muhongo alisema hayo jana wakati wa kikao chake na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, na kuongeza kuwa leo ndio siku ya mwisho ya kukamilisha shughuli hizo nchi nzima. “Katika hili nasema kweli hakuna mzaha. Hatutanii. Wananchi wamechoka, wanataka umeme.
Mtindo wa kuandikiana barua tena haupo. Ukishindwa , unajiondoa mwenyewe”, alisisitiza. Akijibu hoja za Kandoro kuhusu suala la makaa ya mawe, alisema atahakikisha suala hilo linapata ufumbuzi wa haraka kwa kuhakikisha rasilimali hiyo inatumika kama chanzo kingine cha kuzalisha umeme nchini.
Aliongeza kuwa, amewaagiza wawekezaji wote wa makaa ya mawe wenye leseni kukutana naye katika ziara, ili kukubaliana kuhusu suala hilo. Kuhusu matatizo ya maji katika vyanzo vya uzalishaji umeme, Muhongo aliiagiza Tanesco Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kuhakikisha inaandaa kikao cha Wakuu wa Mikoa ya Njombe, Iringa, Morogoro na Mbeya ili kufanya tathmini ya utumiaji maji bila kuathiri pande zote, ikiwemo kutumika kwa ajili ya umeme na kilimo.
“Najua maji yanahitajika sana katika kilimo hususan cha umwagiliaji ambacho ndio cha kisasa. Lakini, hata nishati inahitaji maji. Nawaomba kutaneni zungumzeni halafu tembeleeni maeneo ya mabonde na mashamba mpate taarifa zote, mkimaliza tuangalie suala la kisera linasemaje” .
0 comments:
Post a Comment